Karibu Katika mtandao wa Shirika la Cartoon Forum Tanzania, katika mtandao huu utapata kujua mambo mengi kuhusiana na Shirika hili pia kupata matukio, picha na katuni mbalimbali zenye kuelimisha. Hivyo ni nafasi yako kujifunza na pia kutoa maoni yako, KARIBU SANA...

Thursday, December 21, 2017

Rushwa ya ngono kwa wasichana wa kazi huzalisha madanguro 

Na Adam Malinda, Kwa hisani ya Cartoon Forum Tanzania.

TUNAPOZUNGUMZIA rushwa, zipo za aina mbalimbali katika jamii, zote zinaleta athari kubwa kiuchumi na kijamii, lakini pia huleta athari katika vizazi vya sasa na vijavyo, rushwa hii isipodhibitiwa italitokomeza taifa na kupoteza utu wa mwanamke.


Rushwa ya ngono ni chanzo kikubwa cha mparaganyiko wa maisha ya wanawake, kuanzia majumbani hadi ofisini, jambo hili limekuwa gumu kudhibitika kwa kuwa hufanyika kwa faragha, kificho na ujanja mkubwa. Makala hii inaangazia mwanamke ambae hutumikishwa kazi za ndani, hasa tuzungunzie mwanamke ambaye hufanya kazi za ndani kama sehemu yake ya ajira, lakini tusihusishe wana ndoa, kwa kuwa mjadala wa wana ndoa hauhusiani na rushwa hii tunayotaka kuchambua. Mada inasema nani chanzo cha rushwa ya ngono kwa wanawake wanaofanya kazi za ndani, Ukweli ni kwamba historia za kesi nyingi kati nchi yetu zinaonyesha akina baba huwa ndicho chanzo kikubwa. Hii imetokana na sababu mbalimbali za akina mama kuwapa fursa wasichana wa kazi kufanya kazi nyingi hata zile zinazowaweka karibu na baba zao(baba wenye nyumba), lakini pia kwa kiasi kikubwa akina baba kushindwa kuhimili matamanio yao na kujenga tabia ya ubaguzi, hisia isiyo ya kiungwana ya kuwa msichana yule si wa kumzaa, bali ni mtu mwingine kabisa asiye na mahusiano ya kindugu na familia yake. Fikra hizi hufikia kuwajenga akina baba kuanza ushawishi wa kuwalaghai wasichana hao kwa ahadi ya kuongeza mishahara yao kwa siri kwa sharti la kupewa ngono ya kimwili hali tunayoitafsiri kuwa ni rushwa ya ngono. Hali hii imeleta madhara makubwa kwa jamii kwa kuwa wasichana walio wengi hutoka mikoani (Vijijini) ambako kuna hali duni ya kiuchumi, lishe, Afya na elimu na hatua ya kuja mjini kwao huona ni ukombozi mkubwa. Wasichana hao wamekuwa wahanga wa rushwa ya ngono kwa kuwa matarajio yao ni kubadilisha hali zao za kiuchumi na kuzikomboa familia zao, wanapoingia katika mtego wa mshahara wa kima cha chini na kukumbana na ahadi ya kuongezewa mshahara wa siri na baba mwenye nyumba ni kitanzi kinachowawia ugumu kukiepuka. Lakini pia ieleweke wazi za mwizi 40, ipo siku ikitokea mama mwenye nyumba amebaini, baba atakuwa mtu wa kwanza kujitetea kuwa ni shetani na mazingira aliyoyakaribisha msichana mwenyewe kumuingiza katika mtego baba mwenye nyumba. Mama mwenye nyumba atahamaki na kulinda ndoa yake kwa kumuhukumu msichana kwa kumfukuza bila malipo yeyote na asimwambie akimbilie wapi, mara nyingine humfukuza kwa kumtupia nguo nje, kwa vitisho vya silaha kama visu, panga na vinginevyo. Bila kufahamu msichana huyo akimbilie wapi, hujikuta akiingia katika mikono hatari zaidi katika mikono ya wamiliki wa baa, madanguro, hali ambayo huongeza majanga ya kuingia katika matatizo makubwa ambayo huishia kubeba mimba zisizofahamika wenyewe na kuwatupa wachanga jalalani, kuambukizwa magonjwa ya zinaa ukiwemo ukimwi na mengineyo. Jamii inalazimika kufahamu kuwa rushwa ya ngono huleta athari kubwa katika jamii, kiuchumi, kitamaduni kwa vizazi vya sasa na vijavyo, lakini nini kifanyike, sote kwa pamoja tuungane kuzielimisha jamii zetu kupambana kuikataa rushwa ya ngono, kwa kuwa hatima yake ni mbaya zaidi. Hivyo wote kwa pamoja tuchukue hatua sasa ya kupambana na rushwa ya ngono. Mwisho.

No comments:

Post a Comment