Washiriki wa Mkutano wa kupiga vita Rushwa
ya ngono wakionesha mabango yenye ujumbe wa vita hiyo.
Rushwa ya ngono sehemu za kazi huondoa heshima ya utu, hupunguza tija.
Na Adam
Malinda,
Kwa Hisani
ya Cartoon Forum Tanzania.
RUSHWA ya ngono ni aina mojawapo ya rushwa ambazo
zimeleta athari kubwa katika Jamii hasa
katika maeneo ya kazi, baadhi wameshindwa kuichukia kwa kutokujua, wengine kwa
kutofahamu namna inavyodhalilisha utu wa mtu, lakini baadhi yao kwa kutofahamu
namna ya kupambana na changamoto inayowakabili ambayo ni kujiamini na kusimamia
kile wanachokiamini.
Tunapozungunzia
rushwa ya ngono sehemu za kazi maana yake imeleta unyanyasaji, ukatili na
kunyimwa haki ya mfanyakazi mwenyewe, pale anapostahili mwanamke kupandishwa
cheo, kuongezewa mshahara, kulipwa malupulupu stahiki, kuendelea kazini,
kuepuka kupunguzwa na masuala mengineyo kama hayo.
Mwanamke ni
muathirika namba moja wa rushwa ya ngono kwa sababu ya historia ya mfumo dume
uliojengeka miongo na karne kadhaa zilizopita, ambapo Mwanamke amechukuliwa kama
chombo cha kumtumikia Mwanaume.
Kilio na
masikitiko makubwa katika ofisi za umma na binafsi ni Wanaume kuwa na mamlaka
za juu na kuwaweka baadhi ya wanawake kama makatibu mukhtasi, wanaoongoza idara
za chini, jambo ambalo baadhi ya wanawake walinyanyaswa kijinsia kwa kutoa
rushwa za ngono kwa masharti ili wabaki kazini.
Tatizo
kubwa ambalo limechangia hali hiyo ni usiri wa kitendo hicho na mbinu
zinazotumika kumfikisha mahali pagumu Mwanamke kiasi cha kuamua, “amtumikie
kafiri apate mradi wake “.
Wapo
baadhi ya wanaume nao wamekumbana na
rushwa za ngono kwa mazingira ambayo walishawishiwa kufanya mapenzi ili waweze
kitimiza matakwa yao ya kimaisha, lakini rushwa hii pia imekuwa ngumu
kuthibitika ambapo pia malalamiko ya namna hiyo wanaume wameyachukulia ni aibu
kuliko ilivyo kwa wanawake.
Jukumu
lililopo kwa sasa wanajamii wajenge hisia za utambuzi kwa kuichukia rushwa hii,
kujitambua thamani ya uhuru wa mawazo, utu, na maamuzi makini, kwani kufikiri
kwa njia rahisi, hutatua matatizo kwa njia ya mkato, kukata tamaa, husababisha
kuingia katika mitego ya rushwa za ngono ambazo hupoteza haki ya msingi na utu
wa mtu.
Jamii
ilichukulie suala la rushwa ya ngono kama chukizo linalobeba dhambi kama
zilivyo rushwa nyingine kwa kuwa madhara yake ni makubwa, kwa mfano
unapoanzisha mahusiano sehemu ya kazi,
uwajibikaji hupungua, upendo na mtazamo miongoni mwa mashirikiano na
wafanyakazi wenzako hupungua, kuanza kufanya kazi kwa majungu badala ya umahili,
lakini pia huwapunguzia ari wafanyakazi wenzako, mkuu wa kazi hupoteza heshma
anayostahili kuwa nayo, lakini pia ni udhalilishwaji mkubwa hasa kwa mwanamke
aliyekubali kurubuniwa na kujikuta ameangukia katika mtego wa rushwa ya ngono.
Kwa hakika jamii nzima inapaswa kusema Hapana
kwa rushwa ya ngono ili kurudisha utu wa mwanamke sehemu za kazi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment